ManSillah

TARUMBETA

Waungwana blogspot spousoured by Tarumbeta.

TARUMBETA

Waungwana blogspot spousoured by Tarumbeta.

TARUMBETA

Waungwana blogspot spousoured by Tarumbeta.

TARUMBETA

Waungwana blogspot spousoured by Tarumbeta.

TARUMBETA

Waungwana blogspot spousoured by Tarumbeta.

Wednesday, 17 May 2017

SIMULIZI YA KWELI

Image result for POOR MAN
HUWA YANATOKEA
Kwa jiji la Dar es Salaam, kuanzia majira ya saa kumi alasiri hadi kufikia kumi na mbili magharibi, usafiri hugeuka bidhaa adimu; daladala hazipatikani kwa wepesi, na zikipatikana ni nadra kama si muhali kabisa kupata nafasi ya kuketi; na ikitokea muujiza ukapata nafasi, joto kali pamoja na hewa hafifu, hukufanya utamani kushuka na kutembea kwa miguu. Hiyo ndiyo sababu iliyonilazimu jana, kama nifanyavyo siku nyingine, kutembea kwa miguu badala ya kupanda daladala kama ilivyo ada.
Siku haikuwa njema kwangu; huko kazini nilihitilafiana na bosi wangu, ambaye kwa muda mrefu tumekuwa tukihasimiana na kusigana mara kwa mara, na hatimaye kufikia hiyo jana nilipewa rasmi barua ya kufukuzwa kazi. Ukiwa na familia inayokutegemea kuyakimu maisha, utaelewa ni hali gani nilikuwa nayo hiyo jana. Sasa, nikiwa nimefika maeneo ya Ilala boma, nikirejea nyumbani hali mawazo yakipishana kichwani, mara niliisikia simu yangu ya kiganjani ikiita mfukoni, upesi nikaitoa nikijifariji kuwa huenda kuna maamuzi mapya yamepitika huko kazini, walakini, haikuwa hivyo. Nilipoliona jina la mpigaji, Mbaruda, badala ya kupokea, nilijikuta nikisonya na kuikata, kisha nikairejesha mfukoni huku nikiendelea kupuyanga.
Kwakifupi, Mbaruda ni kijana wa hirimu yangu, niliyehitimu pamoja naye, darasa la saba huko mkoani Tabora. Hatukuwa na usuhuba mkubwa wakati ule wa shuleni, walakini tulipokutana katika mji huu wa ugenini, tulilakiana kwa furaha na buraha, na tukabadilishana namba za simu na kuanza kuwasiliana. Kilio kikubwa cha Mbaruda kwangu ilikuwa ni kazi, hali yake iliyumba kiuchumi, kwa hivi, aliniomba nimtafutie kazi, nami nikaahidi kumfanyia mipango, nikiamini kuwa endapo fursa itatokea hapo kazini kwangu, urefu wa mkono wangu ulitosha kumpachika.
Kwakuwa awashwaye ndiye ajikunaye, kazi ya kufuatilia endapo nafasi ya kazi imepatikana ikawa yake, kwa kunipigia simu kila uchao hadi ikawa kero kwangu. Kilichopelekea nione kero ni ukweli kwamba, tayari kazini kwangu nilikwishaingia kwenye msuguano na bosi wangu, kwa hivyo, ahadi yangu kwake haikuwa yenye kutekelezeka tena, nikawa sipokei kabisa simu zake. Baada ya kupiga simu muda mwingi bila kujibiwa, yamkini Mbaruda alichoka, hakunipigia tena kwa zaidi ya miezi mitatu, hadi kufikia hiyo jana nilipoona tena jina lake kwenye kioo cha simu yangu. Hebu pata picha mwenyewe, kabla tu sijafukuzwa kazi sikumpokelea simu yake kwa kukosa cha kumwambia, sasa nimekwishafukuzwa rasmi, lau ningalipokea, kipi ningalimjibu?
Mguu mosi, mguu pili, nilijiburuza nikiendelea na safari yangu. Nilipofika maeneo ya Buguruni sokoni, mkabala na kituo cha Polisi, ndipo nilisikia mtu akiniita kwa sauti kali, “Mbavu!”
Niligeuka na kuangaza huku na kule, kwa bahati nikamwona mtu ndani ya daladala akiniita kwa kunipungia mkono. Kutokana na magari kusimama kwa sababu ya foleni, niliweza kumfikia mtu yule kabla daladala hazijaanza kundoka. Nilimtambua, jina lake Kinyogori, naye ni kijana mzawa wa Tabora. Baada ya kujuliana hali, yeye akiwa kwenye dalala ilhali mimi nimebarizi kwa nje, usawa wa dirishani, alinihoji kwa wahka, “Mbona haupokei simu kaka, wiki yote hii Mbaruda anakutafuta. Iko hivi, mirathi ya marehemu baba yake ilitoka, na baada ya kuchukua mamilioni yake amenunua kampuni kubwa, na wewe ndiye alikuwa anakutazamia uwe meneja wake!”
Nilihisi jasho likiambaa kwenye uti wa mgongo, kiwewe kilinivaa, nikapoteza mhimili wa kujiamini. Sikuwa na jibu la kumpa Kinyogori, zaidi ya kumdanganya, “Mungu wangu! Nilikuwa safarini kaka, hivi ndiyo nimerudi leo.”
“Duh, nd’o basi tena, haikuwa bahati yako, maana leo ndiyo mwisho wa kuajiri, nimewasiliana naye muda si mrefu, akaniambia amefika maeneo ya Ilala boma, anawahi ofisini, ana miadi na kijana mwingine kwa ajili ya kutiliana naye saini kama meneja wake!”
Kusikia majibu hayo, nilitamani kukaa chini na kulia. Majonzi ya kufukuzwa kazi, ni kama yalishajihishwa na taarifa zile mpya. Kwa vyovyote vile, endapo Mbaruda muda si mrefu alitoka kuongea na Kinyogori akiwa maeneo ya Ilala boma, nami alinipigia simu nilipokuwa mitaa hiyohiyo, bila shaka aliniona kabla hajanipigia, na kama hivyo ndivyo, yamkini aliniona nikiitoa simu na kuikata kabla ya kuirejesha mfukoni. Aibu gani hii! Nitamweleza nini anielewe? Hakika nilitahayari, nilijipotezea bahati kwa ujinga na dharau zangu mwenyewe, nikiamini kuwa Mbaruda ndiye mwenye kunisumbua kwa shida zake. Nikiwa sijapata cha kumjibu Kinyogori, kutahamaki foleni ilifunguka na magari yakaanza kuondoka, tuliishia tu kuagana bila kuhitimisha mazungumzo.
Baada ya hapo, nilirudi upande wa pili wa barabara, nikiwa nimedhamiria kumpigia Mbaruda kumtaka radhi kwa kutompokelea simu, ili nione kama ninaweza kuitwaa fursa hiyo ya kazi. Tazama mipango ya Mungu sasa, kuingiza mkono mfukoni, simu haipo. Nilijipekua kila mfuko bila kuipata, yamkini niliidondosha wakati ule nilipokuwa nikikusudia kuirejesha mfukoni baada ya kuikata simu niliyopigiwa na Mbaruda, au pengine nimeibiwa–balaa juu ya mkosi–nuksi juu ya gundu! Nimepoteza simu pamoja na namba za Mbaruda. Ukisikia kuadhirika ndo huko.
Kwa kihoro na taharuki, nilianza kurejea maeneo ya Ilala boma kwa kasi, huku njia nzima nikipepesa macho kama nitaweza kuiona simu yangu. Fikiria mwenyewe, kwa wingi wa watu barabarani, na kwa muda niliokwisha kutembea, nitawezaje kuipata tena simu hata kama ni kweli nliidondosha! Kupagawa kulinifanya nisiuhisi mchoko wa kutokea Kariakoo hadi Buguruni kwa miguu, niliendelea kurejea kule maeneo ya Ilala boma bila kutafakari mara mbili. Ikumbukwe kuwa, muda huo tayari giza lilikwishaanza kuingia.
Kufika Ilala boma, hamadi, kama Mungu tu, niliikuta simu yangu ikiwa chini, palepale nilipoitoa na kuirejesha mfukoni wakati nilipopigiwa na Mbaruda. Kilichofanya niione kwa wepesi wakati ule wa giza ni mwanga wake, kwakuwa muda huo ilikuwa ikiita. Haraka niliinyakuwa ili nimwone aliyekuwa akinipigia.
Aisee Mungu mkubwa, Mbaruda ndiye alikuwa akinipigia kwa mara nyingine. Kwa yakini, lau kama angaliniona nilipomkatia simu mara ya kwanza, asingalinipigia tena, kwa hivi, itakuwa hakuniona. Nilijifariji kuwa pengine hiyo miadi ya kusainiana na meneja mpya haikufanikiwa, ndipo akarudi kunitafuta tena. Huku mapigo ya moyo yakinienda mbio, nilibonyeza kitufe cha kupokelea, nikaiweka simu sikioni na kupokea kwa taadhima, “Hallow, kaka!”
Kimya!
Ile kusema “Hallow!” kwa mara ya pili, papo hapo nilishituka niko kitandani, na kugundua kwamba nilikuwa usingizini nikiota. Nilikurupuka na kupiga ngumi hewani kwa ghadhabu–haikufaa kitu. Ukweli ulibaki vilevile, kwamba ilikuwa ni ndoto tu, ingawaje ndoto nyingine hubeba maonyo na mazingatio makubwa kwa jamii.