ManSillah

TARUMBETA

Waungwana blogspot spousoured by Tarumbeta.

TARUMBETA

Waungwana blogspot spousoured by Tarumbeta.

TARUMBETA

Waungwana blogspot spousoured by Tarumbeta.

TARUMBETA

Waungwana blogspot spousoured by Tarumbeta.

TARUMBETA

Waungwana blogspot spousoured by Tarumbeta.

Monday, 12 December 2016

KWA NINI WATOTO HUPOTEZA HAMU YA KULA?

KWA NINI WATOTO HUPOTEZA HAMU YA KULA?

Kukosa hamu ya kula ni tatizo la kawaida kwa watoto ambalo hupelekea wazazi wengi kuwa  na wasiwasi juu ya afya ya watoto wao.Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha  kukosa hamu ya kula na tatizo hili linapojitokeza tunatakiwa kuwa watulivu na kujaribu kuchunguza kwa makini ni kwa nini mtoto anakosa hamu ya kula. Baadhi ya sababu zaweza kutatuliwa na mzazi au mlezi lakini sababu nyingine kama zisababishwazo na magonjwa zitahitaji msaada wa wataalam wa afya.

Moja ya sababu kubwa ambayo huwakosesha watoto hamu ya kula ni aina mbalimbali za magonjwa. Magonjwa kama
Malaria, kuhara, maumivu ya tumbo, maumivu ya kichwa, magonjwa ya kinywa na koo, homa na mafua au dalili nyinginezo ambazo humkosesha mtoto raha hupelekea watoto kukosa hamu ya kula.
Matatizo ya kifamilia na msongo ni sababu nyingine ambayo huwakosesha watoto raha na hamu ya kula. Kama walivyo watu wazima watoto pia hukumbana na matatizo ya kifamilia kama kupoteza ndugu au vitu wavipendavyo. Lakini pia watoto hukumbana pia na changamoto mbalimbali za kimaisha kama majukumu ya shule au pengine kukumbana na unyanyasaji kama kuzomewa na mambo mengine mengi yanayokiuka haki zao. Kwa hiyo ili kumuepusha mtoto na ukosefu wa hamu ya kula, wazazi na walezi hawana budi kuwa makini endapo wataona mabadiliko yoyote ya kitabia ya mtoto. Kugundua na kuweza kuziondoa sababu zinazomsababishia mtoto msongo, tutaweza kuwarudisha katika hali ya kawaida na hamu ya kula itarejea tena.
Lakini pia wakati mwingine hali hii hutokana na ugonjwa wa kukosa hamu ya kula ujulikanao kitaalam kama Anorexia nervosa. Watoto wenye ugonjwa huu huweza kukaa muda mrefu bila kula ingawa hawana tatizo jingine, na endapo watapewa chakula huchagua aina fulani tu ya chakula jambo ambalo hupelekea kutopata mlo ulio kamili na hii hupelekea kupungua uzito pamoja na kudhoofu kwa afya zao . Jambo hili linapojitokeza ni vyema kumpeleka mtoto kwa wataalam wa afya wa masuala ya lishe ambao watakuwa msaada mkubwa katika kumsaidia mtoto wako kurejesha tena hamu ya kula.
Kiwango kidogo cha ukuaji wa mtoto huchangia  kupungua kwa hamu ya kula. Katika mwaka wa kwanza wa maisha ya watoto, watoto hukua haraka lakini baada ya mwaka mmoja kiwango cha ukuaji hupungua na kiwango cha chakula wanachokula pia hupungua.Katika wakati huo, hali hiyo ni ya kawaida katika maisha ya watoto.
Sababu nyingine ambazo huchangia watoto kukosa hamu ya kula ni kama maudhi ya dawa, upungufu wa damu, uambukizi wa minyoo na matatizo ya mmeng'enyo mfano mtoto kutopata choo.
Maudhi ya dawa mbalimbali ambazo hutumika kutibu magonjwa kwa watoto yanaweza kuchangia watoto kukosa hamu ya kula. Mfano daktari akimwandikia mtoto dawa za antibiotiki, zaweza kusababisha tazizo la kukosa hamu ya kula. Kupoteza hamu ya kula kwa watoto wanaotumia antibiotiki ni maudhi ya dawa ambayo huwapata watoto wengi. Dawa nyingine pia zaweza kupelekea kupata maudhi ya dawa kama kichefuchefu na kutapika. Tatizo hili humalizika mtoto anapomaliza dawa na endapo atakuwa amepona.
Uambukizi wa minyoo huchangia tatizo hili. Minyoo huingia katika mfumo wa mmeng'enyo wa watoto na kusababisha upotevu wa damu. Minyoo hutegemea ufyonzaji wa damu kama chakula chao, na katika uambukizi sugu hupelekea kuvuja kwa damu,upungufu wa damu, kuhara,kichefuchefu,kutapika na kukosa hamu ya kula. Endapo mtoto ataonyesha dalili za umbukizi wa minyoo, ni vyema kuwaona wataalam wa afya ili kuweza kufanyiwa vipimo na kupatiwa matibabu.
Ugonjwa wa upungufu wa damu ambao kwa kitaalam hujulikana kama anemia, husababishia watoto tatizo hili. Kiwango kidogo cha madini ya chuma katika damu, huwapata watoto ambao hawapati lishe ya kutosha yenye madini haya. Lakini pia anemia yaweza kusababishwa na uambukizi wa minyoo au hata magonjwa mengine. Watoto wenye anemia huwa wadhaifu na wasio wachangamfu, na kama ugonjwa usipotibiwa utaathiri afya ya mtoto hata maendeleo yake shuleni. Ni vyema mtoto akafanyiwa vipimo vya damu endapo utahisi au ataonyesha dalili za ugonjwa wa anemia.
Kwa watoto hasa wadogo, kukosa choo hupelekea kukosa hamu ya kula. Kwa hiyo inapotokea basi ni vyema kupata msaada wa wataalam ili mtoto aweze kuondokana na tatizo hilo.
Wazazi na walezi wazingatie yafuatayo ili kuboresha hamu ya kula ya watoto wao:
  • Kuwa na ratiba nzuri ya kumpa mtoto chakula, na mtoto apewa chakula anapokuwa na njaa.
  • Usiwagombeze au kutoa maonyo makali kwa watoto wakati wa kula.
  • Kuwa na milo midogo kati ya milo mikubwa.
  • Mpe mtoto kiasi kidogo cha chakula lakini mara nyingi kwa siku na siyo kumshindilia kwa wakati mmoja.
  • Usimlazimishe mtoto kula kama hana njaa.
  • Hakisha mtoto anashiriki katika michezo, kwa kuwa michezo huusisha matumizi ya nishati ya mwili na kuboresha mifumo mbalimbali ya mwili.
  • Wakati mwingine mpe nafasi mtoto wa uchaguzi wa chakula akipendacho, lakini chini ya uangalilizi wa mzazi au mlezi ili afanye uchaguzi ulio sahihi.

Wakati wote  wazazi na walezi tukumbuke kuwa tatizo la kukosa hamu ya kula ni la kawaida kwa watoto wengi, na tatizo linapojitokeza hatuhitajiki kuwa na wasiwasi kila wakati. Kama mtoto wako ana afya njema, anapata usingizi vizuri na ni mwenye furaha, hauna sababu ya kuwa na wasiwasi. Lakini kama tatizo litaendelea kwa muda mrefu, basi hatuna budi kuonana na wataalam wa afya kwa msaada zaidi.

FAIDA ZA TIKITI MAJI.

FAIDA ZA TIKITI MAJI.

Tikiti maji ni tunda ambalo kisayansi hujulikana kama Citrullus lanatus katika familia ya Cucurbitaceae, ambalo mmea wake hutoa maua na humea kwa kutambaa. Mmea huu ambao hutoa matunda makubwa yaliyo na umbo la tufe au yai, asili yake ni huko kusini mwa Afrika.
Ushahidi wa kihistoria ulionyesha kuwa mmea huu ulilimwa huko Misri tangu milenia ya pili BC, na katika karne ya kumi AD mmea wa tikiti maji ulikuwa umesambaa huko bara Hindi hata Mashariki ya mbali.Lakini hapo badae ulimaji
wake ulifika huko Ulaya ya kusini na kusambaa duniani kote.Tafiti nyingi zimekuwa zikifanyika kujaribu kuzalisha mbegu za tikiki zenye kukabiliana na magonjwa yashambuliayo mmea huu.
Ijapokuwa watu wengi huamini kuwa tikiti maji ni tunda lililo na maji na sukari peke yake, lakini ukweli ni kuwa tunda hili lina aina nyingi ya virutubisho , mfano vitamini, madini na viondoa sumu(antioxidants).
Jedwali likionyesha kiasi cha virutubisho katika gramu 100 za tikiti maji.
Aina ya kirutubisho
Kirutubisho
Kiwango kilichopo
Vitamini
Vitamini A
28µg

Vitamini E
0.0 µg

Vitamini C
8.1mg

Thiamine
0.03mg

Niacini
0.2mg

Vitamini B 6
0.045mg

Folic acid
3mg
Madini
Kalshamu
7mg

Phosphorasi
11mg

Magnesiamu
10mg

Potasiamu
112mg

Munyu (Sodium)
1mg

Chuma
0.2

Zinki
0.1mg

Shaba
0.0mg

Manganizi
0.0mg
Protini muhimu
TRP(Tryptophan)
7.0mg

THR(Threonine)
27mg

ILE(Isoleucine)
19mg

LEU(Leucine)
18mg

LYS(Lysine)
62mg

MET(Methionine)
6mg

CYS(Cysteine)
2mg

PHE(Phenylalanine)
15mg

TYR(Tyrosine)
12mg

VAL(Valine)
16mg

ARG(Arginine)
59mg

HIS(Histidine)
6mg
Mbali na virutubisho vilivyoonyeshwa katika jedwali, tunda hili la tikiti maji pia lina viondoa sumu kama flavonoids, carotenoids na triterpenoids pia kiasi kikubwa cha maji,na virutubisho hivi hulifanya tunda hili kuwa na sifa ya vyakula vyenye faida kubwa mwilini.
Tafiti nyingi zimeonyesha kuwa, kuongeza matumizi ya vyakula vitokanavyo na mimea kama tikiti maji,matunda mengine na mbogamboga hupunguza hatari ya kupata magonjwa, kuboresha maisha na kuongeza umri wa kuishi. Twaweza kuepukana na magonjwa kama uzito mkubwa(obesity),kisukari na magonjwa ya moyo. Ulaji wa vyakula hivi humfanya mtu kuwa na afya njema,ngozi yenye afya,nywele na uzito ulio wa wastani.
Tunda hili lenye lycopene ambayo ni kiondoa sumu(antioxidant) na ambayo hulipa tunda hili rangi ya kupendeza iliyo nyekundu au pink, pia hupatikana katika nyanya na matunda mengine yaliyo na rangi nyekundu.
Tafiti za awali zimeonyesha kuwa watu walao matunda kama tikiti na mengineyo yenye lycopene kwa wingi waweza kuwa na nafasi ndogo ya kupata maradhi ya saratani hususani saratani ya tezi dume. Lakini hapajakuwepo kwa ushahidi ulio thabiti  kuonyesha uhusiano uliopo kati ya saratani ya tezi dume na utumiaji wa matunda yenye lycopene ili kuweza kutambuliwa na mamlaka za chakula na tiba.
Katika utafiti mmoja uliochapishwa mwaka 2013 katika jarida la Kimarekani la shinikizo la damu, ulionyesha ulaji wa tikiti maji kwa watu wazima walio na uzito mkubwa uliweza kupunguza shinikizo la damu la aota (aortic BP).
L-citrulline ni aina ya protini iliyo katika tikiti maji na ambayo hubadilishwa mwilini katika figo na kuwa protini ijulikanayo kama L-arginine. L-citrulline pia huongeza utengenezwaji wa nitric oxide, ambayo hufanya mishipa ya damu kutokukakamaa na kuboresha mzunguko wa damu mwilini na hii ndiyo sababu ya kupungua kwa shinikizo la damu. Tunda hili limejipatia umaarufu kwa wale walio katika ndoa,kwa kuwa nitric oxide huongeza pia mzunguko wa damu katika viungo vya uzazi, kwa hiyo wale walio na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume kwa kiwango kidogo na kati, waweza kufaidika na tunda hili.
Kwa wana michezo ulaji wa tunda hili au juisi yake ni wa faida kubwa kwa kuwa husaidia kupunguza maumivu ya misuli na kuondokana na uchovu kwa haraka baada ya mazoezi au michezo ya kutumia nguvu. Watafiti wanaamini kuwa hii ni kwa sababu ya uwepo wa protini ya L-citrulline katika tikiti maji.
Tikiti maji ni tunda muhimu katika kurekebisha mmeng’enyo. Kwa kuwa  tunda hili limetengenezwa na kiasi kikubwa cha maji na fiba husaidia kuondoa matatizo ya kukosa choo (constipation) na kuboresha mmeng’enyo wa chakula tumboni. Pia kwa kuwa tunda hili lina asilimia 92 ya maji na madini, huwa ni chaguo zuri kwa wagonjwa wenye upungufu wa maji mwilini.
Hatari ya kupata ugonjwa wa pumu ni mdogo kwa wale wanaokula aina fulani ya virutubisho. Katika moja ya virutubisho hivi ni vitamini C ambayo hupatikana katika aina nyingi za matunda na mbogamboga  likiwemo tikiti maji.
Tikiti maji husaidia afya ya ngozi kwa kuwa lina vitamini A na C. Vitamini A husaidia katika ukuaji wa tishu za mwili,zikiwemo ngozi na nywele. Vitamini C husaidia katika utengenezaji wa kolageni mwilini na husaidia kupona haraka kwa tishu zilizo na majeraha ikiwemo ngozi.
Tahadhari
Tikiti maji siyo lishe iliyokamilika peke yake, pia siyo tiba itakayokufanya kuacha kufuata ushauri wa daktari. Ni vema basi kuhakikisha tunakula mlo ulio kamilika ili kujenga afya bora. Tunapopata matatizo mbali mbali ya kiafya ni vizuri pia kuonana na wataalamu wa afya kwa ajili ya utafiti, ushauri na kupata tiba iliyo sahihi.