KWA NINI WATOTO HUPOTEZA HAMU YA KULA?
Kukosa
hamu ya kula ni tatizo la kawaida kwa watoto ambalo hupelekea wazazi
wengi kuwa na wasiwasi juu ya afya ya watoto wao.Kuna sababu nyingi
zinazoweza kusababisha kukosa hamu ya kula na tatizo hili
linapojitokeza tunatakiwa kuwa watulivu na kujaribu kuchunguza kwa
makini ni kwa nini mtoto anakosa hamu ya kula. Baadhi ya sababu zaweza
kutatuliwa na mzazi au mlezi lakini sababu nyingine kama zisababishwazo
na magonjwa zitahitaji msaada wa wataalam wa afya.
Moja ya sababu kubwa ambayo huwakosesha watoto hamu ya kula ni aina mbalimbali za magonjwa. Magonjwa kama
Malaria, kuhara, maumivu ya tumbo, maumivu ya kichwa,
magonjwa ya kinywa na koo, homa na mafua au dalili nyinginezo ambazo
humkosesha mtoto raha hupelekea watoto kukosa hamu ya kula.
Matatizo ya kifamilia na msongo ni sababu nyingine ambayo huwakosesha
watoto raha na hamu ya kula. Kama walivyo watu wazima watoto pia
hukumbana na matatizo ya kifamilia kama kupoteza ndugu au vitu
wavipendavyo. Lakini pia watoto hukumbana pia na changamoto mbalimbali
za kimaisha kama majukumu ya shule au pengine kukumbana na unyanyasaji
kama kuzomewa na mambo mengine mengi yanayokiuka haki zao. Kwa hiyo ili
kumuepusha mtoto na ukosefu wa hamu ya kula, wazazi na walezi hawana
budi kuwa makini endapo wataona mabadiliko yoyote ya kitabia ya mtoto.
Kugundua na kuweza kuziondoa sababu zinazomsababishia mtoto msongo,
tutaweza kuwarudisha katika hali ya kawaida na hamu ya kula itarejea
tena.
Lakini pia wakati mwingine hali hii hutokana na ugonjwa wa kukosa hamu ya kula ujulikanao kitaalam kama Anorexia nervosa.
Watoto wenye ugonjwa huu huweza kukaa muda mrefu bila kula ingawa
hawana tatizo jingine, na endapo watapewa chakula huchagua aina fulani
tu ya chakula jambo ambalo hupelekea kutopata mlo ulio kamili na hii
hupelekea kupungua uzito pamoja na kudhoofu kwa afya zao . Jambo hili
linapojitokeza ni vyema kumpeleka mtoto kwa wataalam wa afya wa masuala
ya lishe ambao watakuwa msaada mkubwa katika kumsaidia mtoto wako
kurejesha tena hamu ya kula.
Kiwango kidogo cha ukuaji wa mtoto huchangia kupungua kwa hamu ya kula.
Katika mwaka wa kwanza wa maisha ya watoto, watoto hukua haraka lakini
baada ya mwaka mmoja kiwango cha ukuaji hupungua na kiwango cha chakula
wanachokula pia hupungua.Katika wakati huo, hali hiyo ni ya kawaida
katika maisha ya watoto.
Sababu nyingine ambazo huchangia watoto kukosa hamu ya kula ni kama
maudhi ya dawa, upungufu wa damu, uambukizi wa minyoo na matatizo ya
mmeng'enyo mfano mtoto kutopata choo.
Maudhi ya dawa mbalimbali ambazo hutumika kutibu magonjwa kwa watoto
yanaweza kuchangia watoto kukosa hamu ya kula. Mfano daktari
akimwandikia mtoto dawa za antibiotiki, zaweza kusababisha tazizo la
kukosa hamu ya kula. Kupoteza hamu ya kula kwa watoto wanaotumia
antibiotiki ni maudhi ya dawa ambayo huwapata watoto wengi. Dawa
nyingine pia zaweza kupelekea kupata maudhi ya dawa kama kichefuchefu na
kutapika. Tatizo hili humalizika mtoto anapomaliza dawa na endapo
atakuwa amepona.
Uambukizi wa minyoo huchangia tatizo hili. Minyoo huingia katika mfumo
wa mmeng'enyo wa watoto na kusababisha upotevu wa damu. Minyoo hutegemea
ufyonzaji wa damu kama chakula chao, na katika uambukizi sugu hupelekea
kuvuja kwa damu,upungufu wa damu, kuhara,kichefuchefu,kutapika na
kukosa hamu ya kula. Endapo mtoto ataonyesha dalili za umbukizi wa
minyoo, ni vyema kuwaona wataalam wa afya ili kuweza kufanyiwa vipimo na
kupatiwa matibabu.
Ugonjwa wa upungufu wa damu ambao kwa kitaalam hujulikana kama anemia,
husababishia watoto tatizo hili. Kiwango kidogo cha madini ya chuma
katika damu, huwapata watoto ambao hawapati lishe ya kutosha yenye
madini haya. Lakini pia anemia yaweza kusababishwa na uambukizi
wa minyoo au hata magonjwa mengine. Watoto wenye anemia huwa wadhaifu na
wasio wachangamfu, na kama ugonjwa usipotibiwa utaathiri afya ya mtoto
hata maendeleo yake shuleni. Ni vyema mtoto akafanyiwa vipimo vya damu
endapo utahisi au ataonyesha dalili za ugonjwa wa anemia.
Kwa watoto hasa wadogo, kukosa choo hupelekea kukosa hamu ya kula. Kwa
hiyo inapotokea basi ni vyema kupata msaada wa wataalam ili mtoto aweze
kuondokana na tatizo hilo.
Wazazi na walezi wazingatie yafuatayo ili kuboresha hamu ya kula ya watoto wao:
- Kuwa na ratiba nzuri ya kumpa mtoto chakula, na mtoto apewa chakula anapokuwa na njaa.
- Usiwagombeze au kutoa maonyo makali kwa watoto wakati wa kula.
- Kuwa na milo midogo kati ya milo mikubwa.
- Mpe mtoto kiasi kidogo cha chakula lakini mara nyingi kwa siku na siyo kumshindilia kwa wakati mmoja.
- Usimlazimishe mtoto kula kama hana njaa.
- Hakisha mtoto anashiriki katika michezo, kwa kuwa michezo huusisha matumizi ya nishati ya mwili na kuboresha mifumo mbalimbali ya mwili.
- Wakati mwingine mpe nafasi mtoto wa uchaguzi wa chakula akipendacho, lakini chini ya uangalilizi wa mzazi au mlezi ili afanye uchaguzi ulio sahihi.
Wakati wote wazazi na walezi tukumbuke kuwa tatizo la kukosa hamu ya
kula ni la kawaida kwa watoto wengi, na tatizo linapojitokeza
hatuhitajiki kuwa na wasiwasi kila wakati. Kama mtoto wako ana afya
njema, anapata usingizi vizuri na ni mwenye furaha, hauna sababu ya kuwa
na wasiwasi. Lakini kama tatizo litaendelea kwa muda mrefu, basi hatuna
budi kuonana na wataalam wa afya kwa msaada zaidi.