Na Bakari Kimwanga, DODOMA
TUHUMA nzito. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kudai wabunge wote CCM) wamehongwa kila mmoja Sh milioni 10.
Amesema mgawo wa fedha hizo, uliratibiwa vyema na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kushirikiana na Katibu Msaidizi wa wabunge wa CCM, Abdallah Ulega.
Alisema lengo na kutoa fedha hizo ni kutaka kuwalainisha wabunge hao ili wapitishe Mpango wa Maendeleo ya Taifa na Muswada wa Sheria ya Huduma ya Habari unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni leo.
Hoja hiyo aliibuka jana bungeni wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu.
Mbowe alikuwa mbunge wa kwanza kupewa nafasi ya kumwuliza swali Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa lakini Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson alikataa lisijibiwe kwa madai si swali la kisera.
Baada ya kuzuiwa swali hilo, uliibuka mvutano mkali kati ya Mbowe na Dk. Tulia kumpa nafasi mbunge mwingine ili aendelee kuuliza swali jingine.
“Mheshimiwa Naibu Spika, wabunge na mawaziri ni viongozi wa umma kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995. Kuna taarifa ya kwamba siku ya Jumanne Oktoba 25, mwaka huu saa mbili usiku kiliitishwa kikao cha wabunge wa CCM na wewe ukiwa mwenyekiti (Waziri Mkuu Majaliwa), katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana.
“Pamoja na mambo mengine Muswada ambao unatarajiwa kuletwa bungeni kesho (leo) wa mambo ya habari na Mpango wa Taifa ambao tunaendelea kuujadili ulijadiliwa pamoja na mambo mengine yote kikao kile kiliamua kutoa zawadi kwa wabunge wa CCM,wakiwamo mawaziri kiasi cha Shilingi milioni 10 kwa kila mbunge wa CCM wakiwamo mawaziri.
“…zimetolewa kwa viongozi ambao wanabanwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na vilevile mgao huu umeendelea kutolewa ofisi za CCM makao makao, ukiratibiwa na Naibu Katibu wa wabunge wa CCM ambaye pia ni mbunge, Waziri Mkuu taarifa hizi ni za kweli?,” alihoji Mbowe.
Hata hivyo, swali hilo liligonga mwamba, baada ya Dk.Tulia kumzuia Waziri Mkuu kujibu akisema swali hilo lilikuwa kinyume na maudhui ya kipindi hicho.
“Maswali kwa Waziri Mkuu ni maswali yanayohusu sera, waheshimiwa wabunge tukumbushane tu vizuri mheshimiwa Mbowe naomba swali lako liwe linahusu sera.
“Mheshimiwa Mbowe, mimi nitamruhusu kujibu maswali yanayohusu sera kama ambavyo nitamzuia mtu mwingine yoyote kwa hiyo, wewe ndiyo maana nimekupa nafasi tena ili uulize swali linalohusu sera ndivyo kanuni zetu zinavyosema,” alisema.
Licha ya hali hiyo, Mbowe aliendelea kushikilia msimamo wake na kutaka swali hilo lijibiwe kwa kuwa linahusu sera.
“Sijasema tuhuma hizi ni za kweli ila nimeuliza Waziri Mkuu atujibu ni za kweli au si za kweli Naibu Spika unalinda nini?,” alihoji.
Mnyukano kati ya Mbowe na Dk. Tulia, ulimfanya kiongozi huyo wa Bunge kulizuia swali hilo.
“Mheshimiwa Mbowe nadhani hapa tulipofika kama wewe unaona hili swali ni la sera, kanuni hizi ndiyo zinaniongoza mimi kwa maana hiyo nitaendelea na maswali mengine. Mheshimiwa Munde Tambwe Abdallah atauliza swali kwa Waziri Mkuu,” alisema Dk. Tulia.
Hata hivyo, swali hilo lilibuka na kuombewa mwongozo na Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema), ambaye alitaka kujua hatua ya swali hilo kuzuiwa na kama Bunge litakuwa linaona haliwezi iridhiwe ili iundwe Tume ya Kimahakama ili kuchunguza swala hilo.
Mbali na Silinde, pia Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), alimtaka Mbowe athibitishe madai hayo kwani ni masuala yanayohusu vyama na si Bunge huku akisistiza hakuna fedha iliyogawiwa na chama.
Mbowe na wanahabari
Baada ya kipindi cha maswali na majibu Mbowe, alizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa Rais Dk. John Magufuli, amtumbue Waziri Mkuu Kassim Mjaliwa kama anavyowatumbua watendaji wengine.
Alisema taarifa walizonazo katika kikao cha wabunge wa CCM Oktoba 25, mwaka huu, baada ya Serikali kuona hasira za wabunge wao dhidi ya kudorora kwa uchumi, Kinana na Majaliwa walikubaliana kuwapa fedha wabunge.
Alisema tuhuma hizo ni nzito na Bunge haliwezi kujichunguza lenyewe hivyo ni lazima iundwe tume huru ya kimahakama kuchunguza jambo hilo.
“Kwa nchi zilizoendelea jambo hili lingefanya Serikali ijiuzulu leo rushwa ya Shilingi bilioni 2.7 inatolewa kwa malekezo ya kiongozi mkuu wa nchi?…hii ni hatari na inaonyesha tusivyo na utawala bora,” alisema .
Alisema kwa mara ya kwanza wameshangazwa na uamuzi wa Naibu Spika, Tulia Akson, kuwazuia wasitoe ushahidi ndani ya Bunge wakati mara kwa mara wamekuwa wakitakiwa kutoa ushahidi bungeni.
Lissu na barua kwa JPM
Naye Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema alisema watamwandikia barua Rais Dk. Magufuli, kueleza uovu uliofanywa na Waziri Mkuu, mawaziri na Katibu Mkuu wa CCM.
“Tutamwandikia barua kumtaka awatumbue watu wake wa karibu, hizi tuhuma za rushwa ni kubwa na hazipaswi kufumbiwa macho, lazima Bunge lijijengee heshima badala ya kuwa muhuri wa serikali,” alisema
Ulega ajibu
Akizungumza tuhuma hizo Naibu Katibu wa Wabunge wa CCM, Abdallah Ulega, alikiri kufanyika kwa kikao hicho cha Caucas (kokasi), katika Ukumbi wa White House mjini hapa ambacho kilikuwa kinajadili utekelezaji wa bajeti katika robo ya kwanza ya mwaka.
“Ni kweli tulikaa kikao,hakuna shilingi moja aliyopewa mbunge na pale tulikuwa tunajadili utekelezaji wa bajeti katika robo ya kwanza ya mwaka. Katika hili wote tunajua Serikali ilikuwa hajapeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo.
“Hawa wanaoibuka na madai ya ajabu ni wazi sasa wanaonyesha kufilisika kisiasa na wamebaki wanaokoteza hoja mitaani ambazo hazina ukweli. Hivi kwa Serikali hii ya Rais Magufuli pesa ya kuchezea unaitoa wapi,” alisema na kuhoji Ulega.
TAKUKURU
Kutokana na tuhuma hizo za rushwa kwa wabunge MTANZANIA ilimtafuta Mkurugezi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Valentino Mlowola, kuzungumzia tuhuma zilizotolewa na Mbowe.
“Mbowe ni mbunge na Kiongozi wa Kambi ya Upinzania ni mtu ‘senior’ anafahamu taratibu za kisheria hivyo kama ana taarifa na ushahidi chombo kinachoweza kufanya kazi hiyo ni Takukuru, tutamshukuru sana akishirikiana na sisi ili tuweze kuchukua hatua kwasababu tunalipwa kwa kazi hiyo,” alisema.
0 comments:
Post a Comment