NASAHA ZA BABA MWENYE BUSARA
1. Mwanangu, mwanamke anaweza kuwa mkeo, mwingine anaweza kuwa
mama wa watoto wako, lakini ukipata mwanamke ambae atakuwa kama
mama kwako, mama kwa wanao na mama kwa familia, tafadhali mwanangu
usimuache huyo!
2. Mwanangu, usimfanye mwanamke wako kuwa ndio wa kupika na kufanya kazi zote za jikoni peke yake, tabia hiyo sio nzuri Kwani hata nyakati zetu, mashamba yetu yalijulikana kwa majina yetu wanaume lakini tulifanya kazi pamoja!
3. Mwanangu, nikikwambia wewe ni kichwa cha familia, simaanishi kutuna
kwa pochi lako, usiangalie kabisa pochi yako, angalia kama utaona tabasamu usoni kwa mke wako. Pesa sio kila kitu katika ndoa na haileti ukuu wa familia!
4. Mwanangu, ukitaka kuwa na maisha marefu na ukapunguza misongo ya
mawazo, ongea na mkeo pangeni bajeti ya mahitaji yenu, kisha mwache mkeo nawe na jukumu la kuratibu mahitaji ya kila siku ya familia kwa kumkabidhi fungu husika hata kama limetokana na michango yenu wawili. wanawake wanajua sana kupanga bajeti na hii haitakuwa rahisi kwa yeye kutumia hela hovyo wakati akijua kuwa nyumbani kuna mahitaji ya msingi,
lakini hela zikiwa mikono mwako ataendelea kuomba hata kama utakuwa
umeishiwa!
5. Mwanangu, Usithubutu kumpiga mkeo, maumivu ya kipigo hukaa ndani
ya moyo wake kwa muda mrefu sana na huacha kidonda ambacho hukawia sana kupona. Ni hatari sana kuishi na mwanamke mwenye majeraha moyoni!
6. Mwanangu, sasa unaamua kuoa,kama bado utaendelea kuishi maisha kama ya ubachela na mke wako, sio muda mrefu utakuwa bachela tena. ukioa Badilika anza kuishi maisha ya mke na mume!
7. Mwanangu, zamani,tulikuwa na wake wengi na watoto wengi kwa sababu
tulikuwa na mashamba makubwa na mavuno yalikuwa makubwa, lakini kwa
sasa maisha yamebadilika, kwa hiyo mkumbatie mwanamke wako peke yake kwani hakuna ardhi tena na mahitaji ya watoto ni makubwa sana. Angalia ukubwa wa familia yako!
8. Mwanangu, chini ya mwembe ambao nilikuwa nikikutana na mama yako
inaweza kuwa ni hoteli kubwa kwa nyakati zenu,lakini kumbuka, kitu pekee tulichoweza kufanya chini ya mwembe ilikuwa ni kukumbatiana pekee.nakushauri ukikutana na marafiki wa kike kikubwa unachoweza
kufanya nao ni kupeana mikono na ikizidi ni kukumbatiana hadharani sio
vinginevyo!
9. Mwanangu, usibadilike mara utakapoanza kupata mafanikio Zaidi, kuliko kuwahudumia hao viruka njia wa mtaani ambao hawajui mmetoka wapi na mkeo, nakushauri utumie na kufurahia mafanikio yako na mkeo ambae aliweza kusimama imara wakati wote wa mapito yenu magumu.
10. Mwanangu, kumbuka unapoanza kusema au kuona mke wako kabadilika, ujue kuwa kuna kitu ambacho ulikuwa ukikifanya umeacha kukifanya. Jitathmini na anza kufanya au kutimiza wajibu wako.
11. Mwanangu, usijaribu kumfananisha au kumlinganisha mke wako na
mwanamke mwingine wa nje, kwani hata yeye anakuvumilia sana na
hajakufafanisha na mwanaume mwingine yoyote huko nje na ndio
maana aliamua kuwa na wewe.
12. Mwanangu, sasa hivi kuna hiki kitu kinaitwa haki za wanawake, sawa,kama mwanamke anasema ana haki sawa na wewe katika nyumba, basi gawanya mahitaji yote ya ndani kwenu katika sehemu mbili zilizo sawa,halafu timiza nusu yako na mwambie atimize nusu iliyobaki.
13. Mwanangu, nilimuoa mama yako akiwa bado kigoli (bikira) na nilikuwa
naenda sana kwao kabla sijamuoa, lakini kutomkuta mkeo bikra kusikufanye umlaumu kuwa alikuwa muhuni, kumbuka wanawake wa enzi
zetu na wasasa ni tofauti, ulimchagua mwenyewe na ukigoli wake hukuujua
kabisa. Usiingize mambo ya kabla ya ndoa kwenye ndoa yenu.
14. Mwanangu, sikuwapeleka dada zako shule kwa kuwa nilikuwa mjinga
kama wazee wengi wa hapa kijijini wasemavyo, tafadhari usifanye ujinga
huu, kwani kiwango cha mafanikio ya wanawake sasa kimefanya wanaume
waonekane ni watu wa kawaida sana na sio muhimu kama enzi zetu.
Ukijaliwa watoto wape elimu.
15. Mwanangu, zamani enzi za ujana wetu, wanawake walikuwa na urembo
wa asili, ingawa siwezi kukudanganya, wengine waliongeza urembo kwa
kujichora hina na hata kutoboa pua na masikio lakini usisahau hawakuonyesha maumbile yao nyeti hadharani kama sasa. Hakikisha mkeo analijua hili!
16. Mwanangu, mama yako na mimi hatuna hisa katika kila kitu kinachoendelea kwenye maisha yenu, jaribuni kutatua changamoto zenu
wenyewe bila kila mara kuja kwetu kuomba usuluhishi. Ndoa ni pamoja na
ukomavu wa kutatua changamoto zenu bila kuziuza kama gazeti kwa kila mtu.
17. Mwanangu,nilimnunulia mama yako kifaa cha kupikia vitumbua ili
aanzishe mradi wa kuuza vitumbua, pia nilimsaidia kununua cherehani yake ya kwanza, tafadhari msaidie mke wako kutimiza ndoto zake kulingana na uwezo wako kama ambavyo unahangaika kutimiza ndoto zako.
18. Mwanangu, usiache kutusaidia mimi na mama yako, utu uzima una
changamoto nyingi sana na Mungu akikujalia utaziona muda ukifika.
Pamoja na kutimiza majukumu yako kama baba wa familia kumbuka pia
bado tunaishi na wewe ni mtoto wetu.
19. Mwanangu, kila upatapo muda wa kusali, Sali na familia yako, kuna kesho ambayo huijui, ongea na MUNGU wako ambae anajua kila kitu kila siku!
20.NAKUTAKIA MAISHA MEMA YA NDOA MWANANGU….NAKUPENDA!
SHARE NA MARAFIKI UPATE ZAWADI.
0 comments:
Post a Comment