Saturday, 15 October 2016
Home »
» SERIKALI YATANGAZA KIMA CHA CHINI MISHAHARA YA KISEKTA
SERIKALI YATANGAZA KIMA CHA CHINI MISHAHARA YA KISEKTA
Serikali imetangaza viwango vipya vya chini vya mishahara kisekta
ambavyo vinatofautiana kati ya sekta moja na nyingine ambavyo ni kuanzia
Sh40,000 hadi Sh400,000 kwa mwezi kuanzia Julai Mosi mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Wizara ya Kazi na Ajira,
Ridhiwani Wema, watakaolipwa kima kidogo zaidi cha Sh40,000 ni
wafanyakazi wa nyumbani ambao wameajiriwa na watu wa kawaida huku
wakiishi kwenye nyumba za waajiri wao.
Kwa upande mwingine, katika viwango hivyo, kima kikubwa katika viwango
hivyo cha Sh400,000 kitalipwa kwa wafanyakazi wa sekta za mawasiliano
zikiwamo kampuni za simu, kampuni za kimataifa za nishati, madini na
taasisi za fedha.
Katika viwango hivyo, mishahara kwa wafanyakazi wa nyumbani walioajiriwa
na watu wa kawaida lakini ambao hawaishi kwenye nyumba za waajiri wao
itakuwa Sh80,000.
“Viwango vya chini vya mishahara kwa wafanyakazi wa nyumbani
walioajiriwa na mabalozi wa kigeni na wafanyabiashara maarufu wanatakiwa
kulipwa Sh150,000 kwa mwezi,” ilisema taarifa hiyo.
Wafanyakazi wa nyumbani walioajiriwa na maofisa wa Serikali watalipwa
Sh130,000 kwa mwezi.
Kima cha chini cha mshahara katika huduma za kilimo ni Sh100,000 na
huduma za afya Sh132,000.
Kwa upande wa wafanyakazi wa vyombo vya habari, posta na usafirishaji wa
vifurushi ‘courier services’, kima cha chini kitaanzia Sh150,000.
Viwango vya chini vya mishahara kwa wafanyakazi wa hoteli za kitalii
kuanzia Julai Mosi, mwaka huu ni Sh250,000, wakati kwa hoteli za kati ni
Sh150,000 na migahawa, nyumba za wageni na baa ni Sh130,000.
Kampuni za ulinzi za kimataifa zitapaswa kulipa kiwango cha chini cha
mishahara cha Sh150,000 kwa wafanyakazi wake sawa na kampuni ndogo za
huduma za nishati. Kampuni ndogo za ulinzi zitatakiwa kulipa Sh100,000.
Kima cha chini kwa wafanyakazi wa sekta ya usafiri wa anga kitakuwa
Sh300,000, sawa na wale wa utoaji na uingizaji wa mizigo. Wafanyakazi
wanaofanya katika sekta ya usafirishaji wa majini, uvuvi na nchikavu
wakitakiwa kulipwa Sh200,000.
Kima cha chini kwa kampuni za makandarasi daraja la kwanza kitakuwa
Sh325,000, makandarasi daraja la pili hadi la nne Sh280,000 na
makandarasi daraja la tano hadi saba Sh250,000.
Wafanyakazi katika kampuni za uuzaji wa magari watatakiwa kulipwa
Sh300,000 na madalali wa bima watalipwa Sh200,000. Kampuni za wachimbaji
wadogo wa madini zitalazimika kulipa mshahara usiopungua Sh200,000 kwa
wafanyakazi wake.
Mishahara ya chini kwa wafanyakazi wa shule za awali, msingi na
sekondari za binafsi ni Sh140,000 huku wafanyakazi wa viwandani
wakipaswa kulipwa Sh100,000.
Taarifa hiyo ya Wizara ya Kazi imesema sekta ambazo hazijaorodheshwa,
wafanyakazi wake watatakiwa kulipwa kuanzia Sh100,000.
0 comments:
Post a Comment